Lugha Nyingine
Nchi za Mashariki ya Kati zalaani kuuawa kwa kiongozi wa Hamas katika mji mkuu wa Iran
Watu wakishiriki kwenye maandamano ya kupinga kuuawa kisiri kwa Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Siasa ya Kundi la Hamas katika mji wa Hebron, kando ya Magharibi ya Mto Jordan, Julai 31, 2024. (Picha na Mamoun Wazwaz/Xinhua)
CAIRO - Nchi za Mashariki ya Kati siku ya Jumatano zimelaani vikali shambulio linalodaiwa kufanywa na Israel lililomuua Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Siasa ya Kundi la Hamas katika mji mkuu wa Iran, Tehran ambapo taarifa ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran imesema kuwa Haniyeh na mlinzi wake wameuawa mapema siku hiyo ya Jumatano wakati makazi yao yaliposhambuliwa, ikiongeza kuwa shambulio hilo bado liko chini ya uchunguzi na matokeo yatatangazwa baadaye.
Jeshi la Israel bado halijatoa maelezo yoyote kuhusu tukio hilo.
Rais wa Palestina Mahmoud Abbas amelaani kumwua kisiri Haniyeh na kusema ni "kitendo cha uwoga na hatua ya hatari," akitoa wito kwa watu wa Palestina "kuungana, kuwa na subira na imara mbele ya Israel," shirika rasmi la habari la Palestina WAFA limeripoti.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imeeleza katika taarifa yake kwamba shambulio hilo ni "kitendo cha kigaidi," na kusisitiza kuwa "kitendo hicho ni kiovu" kinafuatia mfululizo wa mashambulizi ya Israel kwenye sehemu mbalimbali katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na milima inayokaliwa kimabavu ya Golan ya Syria, Lebanon na Iraq.
Katika taarifa yake iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan "amelaani vikali mauaji ya kiuhaini" dhidi ya Haniyeh, akisema kitendo hicho ni "jaribio la kiovu la kuharibu mambo ya Palestina, mapambano ya Gaza, na mapambano halali ya ndugu zetu Wapalestina."
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq imesema, "kitendo hicho cha shambulizi kimekiuka wazi sheria za kimataifa na ni tishio kwa usalama na utulivu katika eneo hilo."
Katika taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imesema kupamba moto kwa uchochezi wa vita wa Israel katika siku mbili zilizopita "kutasababisha mapambano katika eneo hilo kwa njia ambayo italeta matokeo mabaya zaidi ya usalama."
Nchi nyingine kama vile Jordan, Algeria, na Sudan pia zimelaani shambulio hilo.
Watu wakishiriki kwenye maandamano ya kupinga kuuawa kisiri kwa Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Siasa ya Kundi la Hamas katika mji wa Hebron, kando ya Magharibi ya Mto Jordan, Julai 31, 2024. (Picha na Mamoun Wazwaz/Xinhua)
Watu wakishiriki kwenye maandamano ya kupinga kuuawa kisiri kwa Ismail Haniyeh Mkuu wa Ofisi ya Siasa ya Kundi la Hamas katika mji wa Hebron, kando ya Magharibi ya Mto Jordan, Julai 31, 2024. (Picha na Ayman Nobani/Xinhua)
Watu wakishiriki kwenye maandamano ya kupinga kuuawa kisiri kwa Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Siasa ya Kundi la Hamas katika mji wa Hebron, kando ya Magharibi ya Mto Jordan , Julai 31, 2024. (Picha na Ayman Nobani/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma