Lugha Nyingine
Wanasayansi wawili washinda Tuzo ya Nobel ya Fizikia kwa uvumbuzi unaowezesha kujifunza kwa mashine
Tuzo ya Nobel ya Fizikia Mwaka 2024 ikitangazwa mjini Stockholm, Sweden, Oktoba 8, 2024. (Xinhua/Peng Ziyang)
STOCKHOLM - Tuzo ya Nobel ya Fizikia Mwaka 2024 imeenda kwa wanasayansi wawili, John J. Hopfield na Geoffrey E. Hinton, kwa ugunduzi na uvumbuzi wao wa kimsingi unaowezesha kujifunza kwa mashine kwa mitandao ya neva bandia, Akademia ya Sayansi ya Royal Swedish imetangaza Jumanne.
Washindi hao wa mwaka huu wa tuzo hiyo "walitumia dhana za kimsingi kutoka kwenye fizikia ya kitakwimu kubuni mitandao ya neva bandia ambayo hufanya kazi kama kumbukumbu ambata na kupata muundo katika seti za data kubwa," amesema Ellen Moons, Mwenyekiti wa Akadamia ya Tuzo ya Nobel ya Fizikia.
Hopfield anafanya kazi katika Chuo Kikuu cha Princeton na Hinton katika Chuo Kikuu cha Toronto. Walitumia zana kutoka kwenye fizikia kubuni mbinu ambazo ni msingi wa sasa wa kujifunza kwa kiasi kikubwa kwa mashine, academia hiyo imesema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Mitandao bandia ya neva, ambayo sasa ni muhimu kwa nyanja mbalimbali, ina utafiti wa hali ya juu wa fizikia na imekuwa muhimu kwa maisha ya kila siku, huku ikiwa na matumizi kama vile utambuzi wa nyuso za watu na tafsiri ya lugha, Moons amesema.
Moons amesema faida za kujifunza kwa mashine ni kubwa, lakini maendeleo ya haraka ya teknolojia hiyo yamezua wasiwasi kuhusu athari zake za muda mrefu. Amesisitiza kuwa "binadamu wanabeba wajibu wa kutumia teknolojia hii mpya kwa njia salama na kwa kufuata maadili kwa ajili ya manufaa makubwa zaidi ya binadamu."?
Tuzo ya Nobel ya Fizikia Mwaka 2024 ikitangazwa mjini Stockholm, Sweden, Oktoba 8, 2024. (Xinhua/Peng Ziyang)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma