Lugha Nyingine
Mshindi wa Miss Rwanda 2022 atangazwa baada ya ushindani mkali
KIGALI – Asasi ya Miss Rwanda inayoandaa shindano maarufu la urembo la Rwanda imehitimisha shindano la Miss Rwanda 2022 kwa Mrembo Nshuti Muheto Divine kuvishwa taji.
Fainali za shindano hilo zimefanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Intare mjini Kigali ambapo warembo 19 walikuwa wakiwania taji hilo baada ya mwezi mmoja wa kukaa kwenye kambi ya maandalizi.
Maswali kadhaa yaliyolenga kupima urembo, uelewa wa mambo na maadili ya kitamaduni ya wasichana yaliulizwa ili kuwapata wasichana kumi bora, tano bora na kisha watatu bora kuwa Miss Rwanda na washindi wengine wawili.
Wasichana hao walijibu maswali yao kwa Kiingereza huku washiriki wakiruhusiwa kujibu katika mojawapo ya lugha tatu zikiwemo Kifaransa, Kiingereza na lugha mama ya Kinyarwanda.
Kwa mujibu wa jopo la majaji sita ambao hasa wanatoka katika tasnia ya habari na burudani, mshindi wa pili katika shindano hilo ni Keza Maolithia huku mshindi wa tatu ni Kayumba Darina.
Shindano la Miss Rwanda linaenda sambamba na tuzo nono kutoka kwa wadhamini kadhaa. Na mwaka huu, mshindi amepewa, miongoni mwa zawadi nyingine, gari jipya aina ya Hyundai kutoka Kampuni ya Hyundai Rwanda.
Wakati huo huo, washindi wa nafasi nyingine kadhaa walipewa zawadi kati ya wasichana hao 19 ikiwa ni pamoja na msichana ambaye alikuwa na mpango bora wa afya ya uzazi, michezo ya mafumbo, mrembo mwenye mwonekano mzuri katika picha, mrembo mwenye vipaji, mrembo anayependwa zaidi, mrembo wa shindano la urithi na mrembo mwenye uvumbuzi.
Zamani wazazi walikuwa wakiwazuia watoto wao wa kike kushiriki Miss Rwanda wakidhani kuwa ingewazuia kuzingatia masomo kwa vile wengi wao ni wasichana wenye umri wa kwenda chuo kikuu.
Wengine pia walidhani wasichana wangepoteza maadili yao ya Kinyarwanda, lakini mambo yamebadilika na ushiriki umeongezeka. Tukio la Miss Rwanda pia limekuwa ni jukwaa muhimu kwa watangazaji bidhaa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma