Lugha Nyingine
Hezbollah yaapa kulipiza kisasi kwa Israel kutokana na kumuua kamanda wake wa kijeshi
BEIRUT - Kiongozi wa Hezbollah Sayyed Hassan Nasrallah ameapa siku ya Jumanne kufanya hatua kali za ulipizaji kisasi kutokana na mauaji ya kamanda wake mkuu wa kijeshi, Fouad Shokor, kituo cha televisheni cha nchini Lebanon cha al-Manar kimeripoti huku kikimnukuu akisema kuwa: "Hii ni vita kubwa, na damu ya watu wetu ni ghali sana. Mauaji hayatapita bila kulipiza kisasi."
"Kulipiza kisasi kwetu kwa mauaji ya kamanda wetu bila shaka kunakuja, na kutakuwa kwa nguvu na chenye athari kubwa. Tunaweza kuchagua kulipiza kisasi kwa kushirikiana na makundi mengine ya upinzani nchini Iran na Yemen au kwa nyakati tofauti," Nasrallah amesema katika hotuba yake hiyo iliyorushwa kwenye televisheni kumkumbuka Shokor wiki moja baada ya kifo chake.
Nasrallah pia ametishia kushambulia viwanda vya kaskazini mwa Israel, kila kimoja kwa mujibu wa Nasrallah, kina thamani ya mabilioni ya dola za Marekani.
"Vyote hivi viko kaskazini mwa Israel; ilichukua miaka 34 kujenga viwanda vyote hivi, lakini inachukua nusu saa kuviharibu vyote," amesema.
Nasrallah amesema Israel imeleta hatari kubwa katika eneo hilo. "Hatari hii haiwezi kukabiliwa kwa hofu na kusita; Waislamu wote lazima wachukue wajibu wao," amesema.
Tahadhari inaendelea katika nchi za Lebanon na Israel kufuatia shambulizi la Dahieh katika vitongoji vya kusini mwa Beirut ambalo lilimuua Shokor na raia wengine saba. Nasrallah ametishia mara kwa mara kulipiza kisasi kwa uhakika na kwenye uchungu kwa shambulizi hilo la Israel.
Mvutano katika mpaka wa Lebanon na Israel uliongezeka Oktoba 8, 2023, kufuatia kurushwa kwa roketi mfululizo na kundi hilo la Lebanon la Hezbollah kuelekea Israel katika kuonesha mshikamano na mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel siku moja kabla. Kisha Israel ililipiza kisasi kwa kurusha makombora mazito kuelekea kusini mashariki mwa Lebanon.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma