Lugha Nyingine
Wanadiplomasia wa China na?Ethiopia watoa wito wa kuanzisha shirika la kimataifa la upatanishi wa migogoro
ADDIS ABABA - Wanadiplomasia wa China na Ethiopia wametoa wito wa kushikana mikono ili kuanzisha shirika la kwanza la kisheria duniani la baina ya serikali kwa ajili ya upatanishi wa migogoro ili kufungua njia kwa Dunia yenye amani na ustawi.
Wito huo umetolewa kwenye shughuli ya kwanza ya mkutano wa Shirika la Kimataifa la Usuluhishi wa Migogoro (IOMed) lililoanzishwa na China, iliyofanyika Jumanne huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, na kuvutia idadi kubwa ya maafisa wa ngazi za juu, wasomi na wanadiplomasia kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Mikataba na Sheria ya Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Ma Xinmin, amesema utatuzi wa amani wa migogoro ya kimataifa ni kanuni ya msingi ya sheria za kimataifa kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
"Baada ya takriban miaka mitatu ya ushirikiano wa pamoja, tumepata maendeleo ya aina yake katika kufanikisha IOMed. Ni kwa fahari kubwa kwamba ninatoa taarifa kwa umma jinsi mpango huu umeendelea kushika kasi, na kuvutia washiriki zaidi na zaidi katika mchakato," Ma amesema.
Kwa kuwa ni mpango unaomilikiwa na Nchi za Kusini, IOMed inatazamiwa kuwa shirika la kwanza baina ya serikali lenye dhamira ya kusuluhisha migogoro ya kimataifa kwa njia ya upatanishi, ambalo linajikita zaidi katika mwito mkali wa jumuiya ya kimataifa wa amani, usalama, haki, usawa, na ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote.
Hadi sasa, IOMed imeleta pamoja nchi 19, kati ya hizo 10 zinatoka Afrika, zikiwakilisha watu zaidi ya bilioni mbili duniani kote, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye mkutano huo.
Negus Kebede, mkurugenzi mkuu wa Mambo ya Nchi za Mashariki ya Kati, Asia na Pasifiki katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia, amesema katika mkutano huo kwamba IOMed itasaidia mataifa ya Afrika na mataifa mengine yanayoendelea kuchangia mbinu bora, kuandaa zana madhubuti za kutatua migogoro ya kimataifa, na kuimarisha mchango wao katika diplomasia ya kimataifa na ujenzi wa amani.
"Nataka kutumia muda huu kuipongeza Jamhuri ya Watu wa China kwa kudhamiria kwake bila kuyumbayumba katika kuwezesha mazungumzo ya rasimu ya makubaliano kuhusu IOMed. Juhudi hizi si tu za kidiplomasia bali ni hatua muhimu za kujenga utaratibu wa dunia wenye amani, ushirikiano na mapatano zaidi." Kebede amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma