Lugha Nyingine
Vifaru vya Israel "vimeingia kwa nguvu" katika kambi ya vikosi vya Umoja wa Mataifa Kusini mwa Lebanon: UNIFIL
Picha hii iliyopigwa Oktoba 7, 2024 ikionyesha moshi uliosababishwa na mashambulizi ya anga ya Israel huko Khiam, Lebanon. (Picha na Taher Abu Hamdan/Xinhua)
BEIRUT - Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon (UNIFIL) kimeripoti Jumapili kwamba vifaru viwili vya Israeli vimeharibu lango kuu la moja ya kambi zake Kusini mwa Lebanon na "kuingia kwa nguvu" kwenye eneo hilo baada ya kuzuia harakati zake siku iliyotangulia.
"Majira ya saa 10:30 alfajiri, wakati wanajeshi wa kulinda amani wakiwa kwenye makazi, vifaru viwili vya Merkava vya Jeshi la Israel viliharibu lango kuu la kambi hiyo na kuingia kwa nguvu. Vifaru hivyo viliondoka dakika kama 45 baadaye," UNIFIL imesema katika taarifa, ikisema kambi iliyo katika eneo la Ramyah kwenye mpaka wa upande wa Lebanon.
Kwa mujibu wa UNIFIL, ukiukaji huo ni sehemu ya ukiukaji wa hivi karibuni wa Israel dhidi ya vikosi na kambi za Umoja wa Mataifa wikiendi iliyopita.
"Majira ya saa 12:40 asubuhi, walinzi wa amani katika sehemu hiyohiyo waliripoti mirindimo mingi ya risasi umbali wa mita 100 kaskazini, ikisababisha moshi mwingi kufuka. Licha ya kuvaa barakoa za kujikinga, walinda amani 15 walipata dalili kama vile kuwashwa kwa ngozi na matatizo ya tumbo baada ya moshi kuingia ndani ya kambi hiyo. Wanapokea matibabu," taarifa hiyo imeongeza.
Aidha, UNIFIL imeripoti kuwa siku ya Jumamosi, wanajeshi wa Vikosi vya Ulinzi vya Israeli (IDF) walizuia harakati muhimu za UNIFIL karibu na kijiji cha kusini-mashariki cha Mays al-Jabal.
"Shambulio lolote la makusudi dhidi ya walinzi wa amani ni ukiukaji mkubwa wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu na Azimio 1701 la Baraza la Usalama," UNIFIL imesema, ikiongeza kuwa "imeitaka IDF kutoa maelezo kuhusu ukiukaji huu wa kushtua."
Tangu Septemba 23, Jeshi la Israel limekuwa likifanya operesheni kali ya anga nchini Lebanon, iliyopewa jina la "Mishale ya Kaskazini,"
Siku ya Jumapili, Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati alilaani mashambulizi hayo. Akijibu kauli ya awali ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ambayo akiutaka Umoja wa Mataifa "kuviondoa vikosi vya UNIFIL kutoka hatarini" kusini mwa Lebanon, Mikati alisema hii "inawakilisha ukurasa mpya wa adui kupuuza uhalali wa kimataifa na maazimio yake husika."
Picha hii iliyopigwa Septemba 22, 2024 ikionyesha gari la doria la UNIFIL huko Marjeyoun, Kusini mwa Lebanon. (Picha na Ali Hashisho/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma