Lugha Nyingine
Dunia yashuhudia?Julai yenye hali joto kali zaidi kuwahi kutokea, ukiwa ni mwezi wa 14 mfululizo kuvunja rekodi
Watu wakifurahia muda wao wa mapumziko katika ufukwe wa Brighton, Uingereza, Julai 19, 2024. (Xinhua)
LOS ANGELES - Mwezi uliopita ulikuwa ni mwezi wa Julai wenye hali joto kali zaidi duniani iliyorekodiwa, ambao ulikuwa kwenye viwango vya juu zaidi vya hali joto kali vya kila mwezi kwa miezi 14 mfululizo, kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa na Idara ya Kitaifa ya Mambo ya Bahari na Anga Hewa ya Marekani (NOAA).
Katika ripoti ya kila mwezi iliyotolewa Jumatatu, wanasayansi kutoka Vituo vya Kitaifa vya Taarifa za Mazingira vya NOAA wamesema kuwa wastani wa joto la uso wa dunia katika mwezi wa Julai ulikuwa nyuzi joto 1.21 juu ya wastani wa karne ya 20 wa nyuzi joto 15.8. Ni Julai yenye hali joto kali zaidi katika rekodi ya kimataifa ya NOAA ya miaka 175 iliyopita.
Halijoto za mwezi uliopita zilikuwa juu ya wastani katika sehemu kubwa ya ardhi ya dunia isipokuwa Alaska, kusini mwa Amerika Kusini, mashariki mwa Russia, Australia na magharibi mwa Antaktika, inasema ripoti hiyo, ikiongeza kuwa Afrika, Asia na Ulaya zimeshuhudia miezi ya Julai yenye hali joto kali zaidi iliyorekodiwa, wakati Amerika ya Kaskazini ilishuhudia mwezi wake wa pili wa Julai wenye hali joto kali zaidi.
Ripoti hiyo imegundua kuwa halijoto ya bahari duniani mwezi Julai ilikuwa ya pili kwa hali joto kali zaidi iliyorekodiwa, ikihitimisha miezi 15 mfululizo yenye halijoto kali zaidi iliyorekodiwa.
Ripoti hiyo pia imeonyesha kuwa halijoto ya uso wa dunia ya mwaka hadi sasa ilikuwa nyuzi joto 1.28 juu ya wastani wa karne ya 20, ikiifanya iwe hali joto kali zaidi ya mwaka hadi sasa duniani kuwahi kurekodiwa.
Kwa mujibu wa Mtazamo wa Nafasi za Hali ya Joto Duniani wa idara hiyo, kuna uwezekano wa asilimia 77 kwamba Mwaka 2024 utakuwa mwaka wenye hali joto kali zaidi iliyorekodiwa na karibu asilimia 100 utakuwa kwenye nafasi tano za juu katika orodha.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma