Lugha Nyingine
Watu takriban 23 wauawa katika shambulizi kutoka angani dhidi ya soko kuu Kusini mwa Khartoum, Sudan
KHARTOUM - Raia takriban 23 wameuawa na wengine zaidi ya 40 kujeruhiwa katika shambulizi kutoka angani dhidi ya soko kuu Kusini mwa Mji Mkuu wa Sudan, Khartoum siku ya Jumamosi, watu wa kujitolea na mashirika yasiyo ya kiserikali ya huko yameripoti.
"Tukio hilo limetokea wakati ndege za kivita ziliposhambulia soko kuu la Al-Souk Al-Markazy mjini Khartoum alasiri ya siku ya Jumamosi iliyopita, kliniki ya dharura ya watu wa kujitolea ya Khartoum Kusini imesema katika taarifa yake jana Jumapili.
Majeruhi "wamehamishiwa katika hospitali za Bashair, Elrazi, na Alraqi kwa matibabu. Wengine wako katika hali mbaya," imeongeza taarifa hiyo.
Hadi sasa hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulizi hilo.
Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan (SAF) vilianzisha mashambulizi makubwa Septemba 26 dhidi ya wanamgambo wa Vikosi vya Mwitikio wa Haraka (RSF) katika mji mkuu, Khartoum, ikiwa ni juhudi zake kubwa katika kipindi cha miezi kadhaa za kurejesha udhibiti wa mji huo, habari kutoka jeshi na mashuhuda wameeleza.
Tangu Aprili 15, 2023, Sudan imekuwa katika mgogoro mkali kati ya SAF na RSF, ukisababisha vifo vya watu takriban 20,000, maelfu ya majeruhi, na mamilioni ya watu kuyakimbia makazi yao, makadirio ya hivi karibuni ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu yanaonesha.?
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma