Lugha Nyingine
Wakivutiwa na uhamaji wa makundi ya wanyama mbugani, safari za kitalii za Wachina kwenda Afrika zaongezeka kwa kasi
Mbuga ya Maasai Mara. (Picha/VCG)
Katika miaka ya hivi karibuni, utalii barani Afrika umeongezeka kwa kasi, na watalii wengi kutoka China wanaonekana kando ya Piramidi za Misri na katika nyanda za mbuga za Kenya. Mwaka huu, nchi za Afrika zikiwemo Misri, Morocco, Kenya, Mauritius, na Tanzania zimekuwa vituo pendwa zaidi vya watalii wa China wakati wa likizo.
Ni kitu gani chenye mvuto barani Afrika kinachovutia sana watalii wa China?
Wastani wa gharama za safari ni Dola za Marekani 4,000-6,000, na wamependa kutazama wanyama kwenye mbuga za Afrika
Wakati akitazama machweo kwenye mbuga, Li Yujiao, kijana kutoka China, alihisi kuwa safari hii ilistahili gharama yake, na kwamba kila mtu lazima atembee Afrika mara moja katika maisha yake.
"Nyakati hizi ni nzuri sana," amesema Li Yujiao.
Kwa safari yake ya kitalii ya siku 8 na usiku 7 nchini Kenya, Li na mchumba wake walichagua huduma ya safari ya kitalii ya kundi la watu wawili, ambayo inagharimu yuan 85,000 (sawa na dola za marekani 11969.81) kwa jumla.
Safari ya kitalii kwenda Afrika kwa ujumla ni ghali, na Li Yujiao ana ufahamu mzuri wa hili. "Kenya ni nchi ya Afrika yenye utalii kamilifu kwa wastani. Hoteli nzuri zina hali ya kusanifiwa vizuri na huduma bora, lakini kwa wastani hoteli hizi siyo nyingi."
Ongezeko la asilimia 90: Idadi ya watalii wa China kwenda Afrika yaongezeka kwa kasi
Gharama kubwa za safari za kitalii, hazijazuia hamu ya Wachina kujionea Bara la Afrika. Takwimu kutoka majukwaa kadhaa ya utalii zinaonyesha kuwa tangu kuanza kwa mwaka huu, idadi ya watalii wa China kwenda Afrika imeongezeka kwa kasi tulivu. Misri, Kenya, Tanzania, na Namibia ni nchi za Afrika zilizokuwa na ongezeko la kasi la kupendwa na watalii Wachina wakati wa likizo iliyopita hivi karibuni ya Siku ya Taifa ya China.
Takwimu za Jukwaa la Mtandaoni la Safari za Watalii, Ctrip zinaonyesha kuwa, tangu kuanza kwa mwaka huu, oda za watalii wa China kusafiri kwenda Afrika zimeongezeka kwa asilimia 91, oda za tiketi za ndege zimeongezeka kwa asilimia 78, na oda za hoteli zimeongezeka kwa asilimia 121 mwaka hadi mwaka.
Xiao Cao, mshauri wa kampuni ya uwakala wa safari za kimataifa za watalii mjini Shanghai amesema: "Mwaka jana, ili kuhimiza kustawisha tena sekta ya utalii, nchi nyingi za Afrika zilirekebisha sera zao za visa, hivyo 'wimbi halisi la kusafiri Afrika' lilianza mwaka huo."
Inafahamika kuwa Kenya imekuwa ikitekeleza sera ya kuingia nchini bila visa kwa watalii wa kimataifa kuanzia mwaka huu, Misri imekuwa ikihamasisha urahisishaji wa kupata visa kila wakati, ikirahisisha taratibu za kuingia nchini, na kuongeza uwekezaji kwenye miundombinu ya utalii.
Kwa sasa, nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikihimiza uboreshaji wa miundombinu ya mawasiliano na usafiri wa kuvuka mipaka na kurahisisha taratibu za visa kupitia kusaini makubaliano ya pande mbili na pande nyingi, yakiwezesha safari za watalii za kuvuka mipaka katika nchi mbalimbali.
Kuanzia Septemba 4 hadi 6 mwaka huu, mkutano wa kilele wa FOCAC 2024 ulifanyika Beijing, ambapo China ilisema wazi kuwa inaunga mkono nchi zote za Afrika zenye uhusiano wa kidiplomasia na China kuwa vituo pendwa vya watu wa China kusafiri nje ya nchi kwa utalii wa makundi, kuhamasisha pande zote mbili kuimarisha mabadilishano na ushirikiano wa utalii ili kusaidia kustawisha sekta ya utalii ya Afrika.
"Katika mazingira hayo, huduma za utalii wa China za kwenda Afrika zinazidi kuwa za aina mbalimbali zaidi, huku kukiwa na kampuni za uwakala wa safari za kitalii na miradi ya utalii, na usafiri rahisi zaidi. Miji kama vile Guangzhou, Changsha, na Chengdu imefungua safari za moja kwa moja za ndege za kuelekea nchi za Afrika zenye vivutio pendwa zaidi na watalii," amesema Lin Chen, katibu mkuu wa kituo cha Utafiti kuhusu Sudan Kusini cha Taasisi ya Afrika ya Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang, China.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma