Lugha Nyingine
China na Zambia zaanzisha muundo wa namna ya kutekeleza makubaliano ya FOCAC
Balozi wa China nchini Zambia Han Jing (kushoto) akizungumza kwenye mkutano wa majadiliano ya wazi uliolenga kutathmini fursa zilizotolewa na Mkutano wa Kilele wa 2024 wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) kwa ajili ya kuimarisha uhusiano kati ya China na Zambia uliofanyika mjini Lusaka, Zambia, Oktoba 18, 2024. (Xinhua/Peng Lijun)
LUSAKA - Ubalozi wa China nchini Zambia umesema kuwa nchi hizo mbili zimeanzisha muundo wa kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa kwenye Mkutano wa Kilele wa mwaka 2024 wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).
"Idara zote husika za Zambia, ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Baraza la Mawaziri, na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, zinashirikiana kwa karibu na ubalozi ili kuhakikisha kwamba muundo huo mwishowe utaleta mabadiliko halisi," Balozi wa China nchini Zambia Han Jing ametoa kauli hiyo kwenye mkutano wa majadiliano ya wazi siku ya Ijumaa uliolenga kutathmini fursa zilizotolewa na mkutano wa kilele wa FOCAC kwa ajili ya kuimarisha uhusiano kati ya China na Zambia.
Amesisitiza kuwa China inazingatia kuchukua hatua madhubuti badala ya maneno matupu na imedhamiria kushirikiana na serikali ya Zambia ili kuhakikisha utekelezaji wa matokeo ya FOCAC.
Balozi huyo wa China amesema kuwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000, FOCAC imekuwa jukwaa la msingi la ushirikiano kati ya China na Afrika na mfano wa ushirikiano wa Kusini na Kusini, akiongeza kuwa kuna ushahidi mwingi wa kuonesha kwamba Zambia imenufaika na FOCAC.
Ameelezea imani yake kuwa mkutano huo wa kilele wa FOCAC wa Mwaka 2024 utasaidia kuongeza maendeleo ya Zambia, akisema kuwa China imedhamiria kuunga mkono Zambia kunufaika kutokana na matokeo ya FOCAC kama vile kuiunga mkono kuboresha mazingira yake ya biashara, kuimarisha msingi wake wa kiviwanda, na kuboresha viwanda vyake.
Kwa upande wake Etambuyu Gundersen, Katibu Mkuu anayeshughulikia Ushirikiano na Uhusiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Zambia, amesema FOCAC imekuwa njia muhimu ya ushirikiano kati ya China na Afrika na mfumo muhimu wa ushirikiano wa Kusini na Kusini.
Gundersen, ambaye ameipongeza China kwa kufanikisha mkutano huo, amesema msaada wa China chini ya FOCAC, unahusisha maeneo mbalimbali huku akisisitiza kuwa kipaumbele cha Zambia ndani ya FOCAC kimejikita zaidi katika ushirikiano wa kiuchumi, ikiendana na kujikita kwa nchi hiyo katika miradi iliyobuniwa kwa ajili ya kuongeza ajira na kuendeleza ukuaji wa uchumi.
Mkutano huo ulioandaliwa na Jumuiya ya Uhusiano wa Kimataifa ya Zambia, umewakutanisha pamoja wataalamu kutoka maeneo ya taaluma na taasisi za washauri bingwa ili kujadili na kubadilishana maoni kuhusu fursa zinazotolewa na mkutano wa kilele wa FOCAC.
Wageni wakihudhuria mkutano wa majadiliano ya wazi uliolenga kutathmini fursa zilitolewa na Mkutano wa Kilele wa 2024 wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) kwa ajili ya kuimarisha uhusiano kati ya China na Zambia uliofanyika mjini Lusaka, Zambia, Oktoba 18, 2024. (Xinhua/Peng Lijun)
Etambuyu Gundersen (kushoto) Katibu Mkuu anayeshughulikia Ushirikiano na Uhusiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Zambia akizungumza kwenye mkutano wa majadiliano ya wazi uliolenga kutathmini fursa zilizotolewa na Mkutano wa Kilele wa 2024 wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) kwa ajili ya kuimarisha uhusiano kati ya China na Zambia uliofanyika mjini Lusaka, Zambia, Oktoba 18, 2024. (Xinhua/Peng Lijun)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma